M-Pesa yarejea hewani
· Tatizo la kiufundi latatuliwa.
· Wateja waombwa radhi, waendelea kuituminia
Dar es Salaam, Tanzania June 18, 2014: Wateja wa huduma ya M-pesa wamehakikishiwa usalama wa fedha zao wakati ambapo huduma hiyo ikiwa imerejea kwa asilimia mia moja baada ya kukosekana kufuatia tatizo la kiufundi lililojitokeza mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kuwa huduma hiyo kwa sasa iko imara na kuchukua nafasi hiyo kuwoamba radhi wateja kwa usumbufu walioupata wakati huduma hiyo ilipokosekana.
“Napenda kuwaomba radhi wateja wetu ambao wamekuwa na wakati mgumu kupata huduma ya M-pesa katika siku chache zilizopita. Tunatambua umuhimu wa huduma hii kwao. Hali iliyojitokeza ilikuwa nje ya uwezo wetu na kamwe hatukulitarajia.”Alisema Meza
Meza amesema kilichotokea kwenye mfumo wa M-pesa ni changamoto ambayo mfumo wowote unaotumia teknolojia unaweza kukumbana nayo bila kutarajia lakini jambo la muhimu ni kwa jinsi gani mtoa huduma anavyoweza kujipanga kuitatua kwa uharaka kudhibiti madhara makubwa zaidi kwa wateja.
“Unapokuwa katika suala la teknolojia chochote kinaweza kutokea ni kama vile inavyoweza kutokea kompyuta kukataa kuwaka lakini cha msingi ni kwa uharaka gani unaweza kudhibiti tatizo na kufikia ufumbuzi, hilo ndilo tulilolifanya na kwa sasa tunayo furaha kwamba wateja wetu wanaendelea kupata huduma.”Aliongeza
Kuhusu usalama wa fedha Meza amewahakikishia wateja wa Vodacom na wabia wake wote wanaoutumia huduma hiyo kwamba fedha zote zipo salama na zinalindwa kwani kilichotokea ni wateja kushindwa kuipata huduma hiyo kwenye menyu za simu zao za mkononi na sio tatizo kwenye mfumo mzima wa M-pesa.
‘Fedha zote zipo salama na zinalindwa. Kama wakati tatizo lilipotokea mteja alikuwa na Sh 1/- au Sh 100/- ,Milioni basi ni kiwango hichohicho atakuwa amekikuta kwenye akaanti yake ya M-pesa au hata ya M-pawa mara baada ya huduma kurejea.”Alifafanua Meza
Meza amewashukuru wateja wa M-pesa kwa uvumilivu na ustahamilivu wao wakati timu ya watalaamu wa ndani na nje ya nchi walipokuwa katika juhudi za kutafuta uvumbuzi wa tatizo lililojitokeza.
“Wateja wetu wamekuwa wavumilivu na wameendelea kuitumia kupitia mawakala zaidi ya 70,000 walioko nchi nzima. Hili unaweza ukaliona kupitia namna ambavyo wateja walivyoendelea kuitumia M-pesa mara baada ya kurejea, tunawashukuru sana na tunaendelea kuwaahidi huduma bora.”Aliongeza
“Hakuna madhara ya kibiashara kwetu, ila kutokana na M-pesa kuwa tegemezi kwa mamilioni ya watanzania katika maisha yao ya kila siku ikiwa ndio huduma kinara ya fedha kwa njia ya simu za mkononi, ni wazi kwamba imeleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji.”
No comments:
Post a Comment