la saba, lakini ameweza kufikia
hapo alipo kwa jitihada zake
mwenyewe.
NA >Herieth Makwetta, Mwananchi
Jina la Flora Lyimo au Mbuta
Nanga limekuwa maarufu katika
mitaa ya Oxford inayosifika kwa
kuwa na wabunifu wakubwa duniani,
jijini London nchini Uingereza.
Hata hivyo, hakuna anayejua
ukweli kuhusu historia ya maisha
ya Mbuta Nanga, Mtanzania
ambaye kwa sasa ni raia halali wa
nchi hiyo. Flora anayemiliki duka
kubwa la mavazi katika mitaa hiyo,
amekuwa kivutio kikubwa kwa
wengi wanaohitaji mavazi ya kibunifu,
hasa kutokana na ucheshi,
pamoja na uzoefu wa kufanya
biashara hiyo kwa muda mrefu.
Haikuwa rahisi kwake kufikia
hatua hiyo kwani historia yake
inaonyesha kwamba, Mbuta Nanga
hakubahatika kusoma kutokana na
wazazi wake kutokuwa na uwezo.
Binafsi anasema kuwa mafanikio
aliyonayo sasa ameyatafuta kwa
miaka 30 hadi kuyafikia.
Katika mahojiano na gazeti hili,
dada huyo anasema kuwa, hakuridhika
na hali halisi ya kimaisha,
hivyo alianza kufikiria namna
atakavyoweza kujiimarisha ili aipe
furaha familia baada ya kumaliza
darasa la saba.
Mwaka 1989 Kijijini Kilema
Marangu
Huku ndiko maisha ya Flora (Mbuta
Nanga) yalikoanzia.
Anasema kuwa baada ya kuhitimu
elimu ya msingi, hakufanikiwa
kuendelea na masomo ya sekondari
hivyo elimu yake ni darasa la
saba mpaka sasa.
“Nimezaliwa katika Kijiji cha
Kilema huko Marangu, Moshi
Kilimanjaro Aprili 23, 1974 katika
familia ya Basilei Pius Lyimo
na Augustina Lyimo. Tumezaliwa
watoto 11, wasichana saba
na wavulana watatu, mimi nikiwa
mtoto wao wa saba ‘lucky seven’
kama nilivyokuta wakisema
Waingereza,” anaanza kusimulia.
Anasema kuwa baada ya kukamilika
kwa muda wa kuanza shule,
alisoma katika Shule ya Msingi
Kilema Kubwa mpaka darasa la
saba na kufanikiwa kuhitimu mwaka
1989.
“Nasikitika kwani hapo ndipo
elimu yangu ilipoishia, kwa kuwa
wazazi wangu hawakuwa na uwezo
wakunisomesha sekondari, japo
nilitamani sana kuendelea na masomo,”
anasema.
Mbuta Nanga anasema kuwa
hakuwa na namna bali kujiandaa
kwenda mjini kutafuta kazi ili arudi
nyumbani kila Sikukuu ya Krisimasi
arudi nyumbani na mabegi
makubwa ya zawadi kama ulivyo
utamaduni wa watu wa Kabila la
MAISHA
Duka la Flora Lyimo TZUK lililopo katika mitaa ya Oxford jijini London, mwezi Desemba mwaka '
huu anatarajia kufungua duka jingine katika mitaa hiyo.
Wachaga tangu enzi hizo mpaka
sasa.
“Kama nilivyokuwa naona watu
wakija kijijini wakati wa Krisimasi
na mabegi nilidhani ilikuwa ni
kazi rahisi. Nilifikiri kwenda mjini
inaimanisha kila Krisimasi ni kurudi
kijijini na zawadi kibao, kumbe
wapi, kuwa ujionee,” anasema.
Anasema kwamba alitamani
kusoma lakini hakuwa na jinsi bali
aliamua kutulia kwanza nyumbani
mpaka atakapopata bahati ya
kutoka. “Kwa kuwa nilikuwa na kiu
ya pesa, nilihisi ipo siku nitamiliki
pesa nyingi kama nitajituma
na hilo hasa lilikuwa lengo langu,”
anasema Mbuta Nanga.
Anafafanua: “Basi mwaka 1990
nilibahatika kwenda mjini kwa
mara ya kwanza, nilichukuliwa
kijijini kwetu kwenda kufanya kazi
za ndani hasa kukaa na mtoto wa
dada mmoja naye ni Mchaga, aliyekuwa
akiishi Nairobi. Alimwambia
mama yangu kwamba nitakuwa
namwangalia mtoto wake mmoja
aliyekuwa naye wakati anakwenda
kazini na akirudi jioni mimi
nitakuwa naenda shule kujifunza
kizungu na kuandika kwa mashine
(computer).”
Anabainisha kuwa haikuwa
rahisi kwa mama yake kukubali
ombi hilo, lakini aliposhawishiwa
zaidi alimkubalia na kumwachilia
aende Nairobi kutafuta maisha.
“Mama yangu akakubali, ndipo
safari yangu ya Nairobi ikaiva.
Nilikaa Nairobi kwa mwaka mzima
na ilipofika Desemba 1990, wakati
wa Sikukuu ya Krisimasi, nikarudi
nyumbani. Kabla ya safari, yule
dada alinikataza kununua vitu na
kuniambia nipeleke pesa nyumbani,
kwani zitamsaidia mama kwa
kuwa sijui anashida gani. Ni mwaka
sasa sijamwona yeye na ndugu
zangu hivyo ni vizuri kwenda na
pesa,” anasema.
Anasimulia kuwa kutokana na
kuhisi ushauri huo unafaa, alikubaliana
naye kwa shingo upande
ili kumridhisha.
“Nilimsikiliza na nikaenda na
kibegi kimoja ambacho sikupenda
kwa kweli, lakini tulienda kufanya
shopping za kila kitu nikiwa na
mama yangu na ndugu zangu wote
walikuwa na furaha kweli, sikukuu
ilipokwisha nilirudi tena Nairobi
kwa yule dada na nikaendelea na
kazi za nyumbani. Kazi yangu ilikuwa
ni kukaa na mtoto wake na
kweli jioni nikaenda shule kujifunza
Kiingereza na kuandika kwa
kompyuta,” anasema.
Kunyanyaswa kijinsia
Mwaka 1991 wakati huo (Flora)
akiwa na umri wa miaka 16 na
alishaanza kubadilika kimaumbile
na kuona mambo mengi ya mjini,
hasa kuhusu ujana lakini hakujishughulisha
nayo.
“Nilianza kupata shida kwa
mume wa yule mama. Kila anapopata
nafasi alikuwa akirudi
nyumbani bila mkewe na kunikuta,
kisha kunipapasa na kutaka nifanye
naye mapenzi. Mimi nilimkatalia,
lakini unyanyasaji huo ulikuwa
unaniumiza moyoni hata nikalia
sana,” anasema.
Mbuta Nanga anasema kulia
kwake hakukumsaidia kwani
jamaa huyo aliendelea kumnyanyasa
kwa kumtaka kimapenzi jambo
ambalo hakuwa tayari na alihisi
hakustahili.
“Niliwahi kumwambia kwamba
ningemweleza dada, hapo akaniomba
nisimwambie akaahidi hatofanya
tena. Tatizo lilikuwa kwamba
kila usiku anapokuja mimi ndiyo
huenda kufungua mlango na dada
(mke wake), anakuwa amelala.
Alikuwa hamfungulii mlango
sababu mumewe alikuwa mlevi
sana. Hivyo kila akirudi amelewa
na hapo huanza kugombana, basi
akanipa mimi hiyo kazi ya kumfungulia
mlango,” anasema.
“Kila akiingia alikuwa akianza
kunishika matiti na huku anataka
kunibusu, basi kimya kimya
nikawa namtoa mikono na kujizuia
ili dada asisikie kwani sikupenda
mimi niwe chanzo cha ugomvi
wao, nilipoona anaendelea hivyo
nikamwambia mama mmoja rafiki
wa dada. Dada akaamua kuniondoa
pale na kwenda kukaa na huyu
mama rafiki yake, huku nikawa
naendelea na shule,” anasema na
kuongeza:
“Kwa yule mama mwingine, yeye
alikuwa na mume ila hana mtoto.
Basi nikawa naenda kanisani kila
Jumapili nilikuwa mapumzikoni.
Huko kanisani nilikutana na akinadada
wafanyakazi za nyumbani
kama mimi, tukawa tunaongea
na kufahamiana. Wengi walikuwa
Watanzania,” anasimulia.
Mbuta Nanga anasema kwa
kipindi kile Kenya kulikuwa na sheria
ya kila mtu kuwa na kitambulisho
cha makazi na cha uraia, lakini
upande wake hali ilikuwa tofauti.
Chakacha yamharibia ajira
Kama una kumbukumbu mwanzoni
mpaka mwishoni mwa miaka
ya 1990, uchezaji wa chakacha
ulikuwa miongoni mwa mitindo
ya kipindi hicho, iliyoteka hadhira
na safari hii Mbuta Nanga alishawishiwa
kuingia huko.
Anasema kuwa Jumapili moja
alikutana na binti mwingine
ambaye alimshawishi waende
wakaangalie shoo sehemu moja
jijini Nairobi.
“Basi tukaenda naye kulikuwa na
msichana mmoja alikuwa anacheza
chakacha na nilipoona anavyocheza
nilifurahi na kusema hata
mimi nitaweza. Yule msichana
akaniambia kama nitaweza basi
niende kucheze, niachane na kazi
za nyumbani.
Tukaenda mimi na yeye na kuuliza
mtu akitaka kucheza kama yule
dada wa chakacha anahitaji nini,
tukaambiwa ni wewe uje mchana
utuonyeshe jinsi unavyocheza
halafu tutakuambia kama unaweza
au la,” anasimulia
Mbuta Nanga anasema kuwa
haikuwa rahisi kwake, lakini alimwomba
kwenda siku ya Jumapili,
ndipo anapopata nafasi na kukubaliwa
kutoka.
Itaendelea wiki ijayo '
No comments:
Post a Comment