MKILETEWA HAPA NA MISS FB-FLORA BAHAT LYIMO" Linda Kapinga: Bunge la Vijana limeniongezea uwezo: |
![]() BY Joseph Kapinga ; Linda Kapinga (22) ni kijana wa kitanzania. Ni mwanafunzi wa Shahada ya Mawasiliano ya Jamii (Mass Communication) katika Chuo Kikuu cha Coventry kilichopo Jijini London Uingereza. Binti huyu wa kitanzania amepata fursa kuhudhuria mkutano wa Bunge la Vijana kwa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola (CommonWealth Youth Parliament). Akiiwakilisha Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi saba za Afrika zilizotuma wawakilishi kwenye bunge hilo. Mwandishi wa gazeti hili amepata fursa ya kufanya mahojiano na kumuuliza pamoja na mambo mengine maazimio ya mkutano huo ambao msingi mkuu ulilenga katika kuwekeza elimu ya siasa kwa vijana ili baadaye waweze kuwa chemchem bora ya mabadiliko ya kisiasa katika nchi zao. Swali: Utaratibu gani unatumika katika kuwapata wawakilishi kwenye mkutano huo, au kwa maneno mengine wewe kama mwakilishi wa Tanzania ulipataje nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mkutano huo? Jibu: Kwa kawaida Bunge la Tanzania ndilo linalochagua mwakilishi kwenda Bunge la Vijana la Jumuiya la Madola. Mimi naishi Uingereza, kupitia ubalozi wa Tanzania nchini humo ndio waliochagua jina langu baada ya kupitia maelezo yangu binafsi (CV). Sifa muhimu ya chaguo ni vijana wenye upendo wa kazi [Charity work], Ujasiriamali [Entrepreneurship], au Ubunifu binafsi wa ziada. Maombi yalikuwa mengi, baada ya kuchujwa tukabaki wawili. Swali: Lengo kuu la mkutano huu lilikuwa nini, na mbali na Tanzania nchi gani nyingine za Afrika zilizoshiriki? Jibu: Lengo kuu la Mkutano huu ulikua sio tu kuwakilisha nchi yako, bali pia kujifunza zaidi kuhusu jinsi Bunge linavyofanya kazi. Msingi mwingine ni kutoa mafunzo na kutayarisha viongozi/wabunge wa baadaye, na pia kutupa nafasi ya kutoa hoja na kuzijadili kutoka kwa wawakilishi wa mataifa mbalimbali. Mbali na hilo, pia tulipata fursa ya kulitembelea mabunge mawili ya Uingereza [House of Lords na House of Commons] kuzoea mazingira. Mbali na Tanzania, nchi nyingine za Afrika ni pamoja na Malawi, Nigeria, Zambia, Uganda, Kenya, Cameroon na Swaziland. Swali: Kama mwakilishi wa Tanzania, wewe binafsi umefaidika na nini? Jibu: Kama Mwakilishi wa Tanzania nimefaidika na vitu vingi sana kwenye huu mkutano. Kubadilishana mawazo na mawakilishi wa nchi nyingine na kujifunza kuhusu sekta mbalimbali. Pia uwezo wangu kifikra umepanua na kuniongezea nafasi ya kujiamini katika maamuzi kama kijana wa kike. Swali: Kwa sasa unaishi Uingereza, je vijana wenzako wa Tanzania watajifunza vipi kutoka kwako kama mwakilishi? Jibu: Kwanza naomba nikumbushe kwamba mimi kuishi Uingereza haimanishi sijui kinachoendelea nchini kwangu. Kama mwakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya la Madola, nataka kuwahamasisha vijana wenzangu wajihusishe kwenye mambo yanayoendelea nchini. Bunge sio la wazazi wetu tu, vijana pia tunapaswa kushiriki kwa vile maamuzi yanayotolewa kwenye vikao yanatuhusu sote. Si lazima na vijana tuingie bungeni na kuongea lakini pia kuuliza maswali na kuhakikisha yanajibiwa, kufuatilia na kuchangia katika jamii. Hivi ni vitu vinavyosaidia kuendeleza nchi yetu. Swali: Inawezekana kabisa kwamba, vijana wengi hawafahamu uwapo wa Bunge hilo la vijana, je, wewe binafsi ulipata wapi taarifa zake kiasi hata cha kuweza kutuma maombi? Jibu: Kujihusisha na mambo yanaondelea kwenye jamii ni moja ya njia ya kujulishwa kuhusu mikutano kama hii. Mimi najihusisha na mambo mengi na naendelea kujihusisha. Nilisikia kuhusu huu mkutano na nikauliza jinsi ya kujiandikisha. Kwa hiyo kama kuna vijana wanaotaka kujua vitu vinavyoendelea, kwanza wanapaswa kuwa wadadisi wa kutaka kujua mambo mengi si tu kwa ajili yao binafsi bali kwa jamii nzima wanayoishi. Fursa za vijana kujiendeleza ziko nyingi, tatizo naloliona kwa vijana wengi kwa nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa mojawapo, ni ukosefu wa ubunifu. Vijana wanataka maendeleo lakini hawataki kujituma, wanangoja maendeleo yawafute walipo. Si jambo linalowezekana. Swali: Kupitia kushiriki kwako kwenye mkutano huo, ni changamoto gani umekumbana nazo ukilinganisha hali halisi ya maisha ya vijana wengi wa Tanzania. Jibu: Mimi ni mzaliwa wa Tanzania na sehemu kubwa ya maisha yangu ilikuwa Tanzania kabla ya kuja hapa Uingereza. Kwa hiyo nimeishi sehemu zote mbili na nimejionea kufanana na kutofanana kwa mambo kadhaa kati ya nchi hizi mbili. Kushiriki kwenye mkutano huu na kukutana na washiriki kutoka nchi mbalimbali na kujifunza zaidi kuhusu nchi zao, mimi kama Mtanzania, kumenifumbua macho na upeo wa uelea kwa kiwango kikubwa zaidi. Napata changamoto ni jinsi gani Tanzania tunahitaji kuendelea kupigania maendeleo yetu hasa kupitia vijana ambao kwa idadi ndio wengi kati ya Watanzania zaidi ya milioni 40. Changamoto nyingine ni kwamba, vijana wenzetu kutoka nchi nyingine wanaonekana kuwa na upeo wa mambo ya Bunge kwa vile serikali zao zinashirikishwa. Nadhani fursa hii haipo kwa vijana wa Kitanzania. Swali: Unawaeleza nini vijana wenzako, hasa wale wa Tanzania ambako ndiko ulikozaliwa? Jibu: Vijana tunahitaji kujihusisha katika vyombo vya kutoa maamuzi. Sio kwa kuingia Bungeni tu, bali pia kuwa na muda wa kuzungumza vizuri na wazazi/wakubwa wetu na kuelewa kinachoendelea nchini. Nawahamasisha vijana wenzangu wajitume zaidi ili kujijenga zaidi. Swali: Nini matarajio yako ya baadaye/binafsi na kikazi? Jibu: Kwa sasa mimi bado nasoma Chuo Kikuu cha Coventry, London nikichukua elimu ya Mawasiliano na Vyomba vya Habari. Mbali ya kuwa mbunifu, nimechagua kusomea Mawasiliano na Vyombo vya habari kwa sababu nia ni kuhamasisha wananchi kutumia vyombo vya habari kujenga umoja na mshikamamo. Mbali ya shule sasa ninajihusisha na makampuni tofauti ya vyombo vya habari hapa Uingereza kama Shirika la Habari (BBC). Matumaini yangu ni kuja kuwa mmiliki wa vyombo vya habari hasa televisheni na radio. Kwasasa najitahidi kuwasiliana na watu mbalimbali ili kuweza kuanzisha/kuendeleza ratiba/mafunzo ya vitendo baada ya shule ili kujenga uwezo wa kujiamini na kuboresha kipaji. |


I love this,Exellent.
ReplyDelete